Switch to App

NDUMBARO ATANGAZA MAGEUZI 15 MAKUBWA YA SHERIA ZA UCHAGUZI CHINI YA UONGOZI WA RAIS SAMIA

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, ametangaza leo juni 9 2025 Tarime Mkoani Mara kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya mageuzi makubwa 15 katika sheria za uchaguzi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha demokrasia na utawala bora nchini.

Akizungumza mjini Tarime, alipokuwa akifungua mafunzo ya elimu ya kisheria kwa viongozi wa kata, Dkt. Ndumbaro amesema mageuzi haya yanadhihirisha dhamira ya kweli ya Rais Samia ya kujenga mfumo huru, wazi na wa haki wa uchaguzi.

Mabadiliko hayo yamejumuisha kufutwa kwa sheria ya zamani ya uchaguzi ya taifa na ile ya serikali za mitaa, na badala yake kutungwa sheria mpya ya uchaguzi inayoendana na matakwa ya sasa ya kidemokrasia.

Kwa mara ya kwanza, Tanzania imepata sheria mahsusi ya Tume Huru ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024, hatua inayolenga kuimarisha uhuru na uwajibikaji wa taasisi hiyo muhimu.

Aidha, nafasi ya Mkurugenzi wa Halmashauri kuwa msimamizi wa uchaguzi imeondolewa, ambapo sasa wasimamizi watapaswa kuomba nafasi hizo na kufanyiwa usaili na Tume Huru.

Katika hatua nyingine, majina ya wasimamizi wa uchaguzi kwasasa yatatangazwa kupitia Gazeti la Serikali na kubandikwa hadharani, huku wale waliowahi kuwa viongozi wa kisiasa ndani ya miaka mitano hawataruhusiwa kushika nafasi hizo.

Wananchi, vyama vya siasa na wadau wengine wamepewa haki ya kuweka pingamizi dhidi ya wasimamizi wa uchaguzi.

Mabadiliko haya yanalenga kuongeza uaminifu wa umma katika mchakato wa uchaguzi na kuondoa mianya ya upendeleo au migongano ya maslahi.

Kwa upande wa haki za kupiga kura, mageuzi haya yanajumuisha pia kuruhusu wafungwa na mahabusu ambao vifungo vyao havizidi miezi sita kujiandikisha na kushiriki katika upigaji kura.

Ili kuwezesha hilo, vituo maalum vya kupigia kura vitaanzishwa ndani ya magereza.

Aidha, uteuzi wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi utafanyika kwa uwazi na kuzingatia sifa, ili kuhakikisha tume hiyo inaendeshwa na watu wenye uadilifu na weledi.